Jinsi ya kuthibiti hasira katika mahusiano

KAMA ilivyo barabara ambayo ina mabonde, milima na mashimo na wakati mwingine kunyooka, ndivyo ulivyo hata uhusiano wa kimapenzi. Hakuna uhusiano wowote usiokabiliwa na changamoto ya mgongano wa fikra, kutofautiana na wakati mwingine hata kugombana na kupandishana hasira.

Pamoja na ukweli huo, zipo njia thabiti zinazoweza kukusaidia kuepuka kuacha hasira zako kukufanya uonekane mtu wa ajabu mbele ya mwenza wako na hata kufikia hatua ya kukuharibia uhusiano wako.

Athari za kuendekeza na kushindwa kudhibiti hasira zako ni kubwa na wakati mwingine zinaweza kukufanya watu wakakaa mbali na wewe na kushindwa hata kujaribu kutafuta suluhu ya tatizo.

Wapo watu kwenye uhusiano hutumia udhaifu huo wa hasira, pindi wanapokorofishana na wenza wao, na kuamua kuchukua hata wiki wamenuna, visirani na wakati mwingine hata kutoa maneno yasiyo na staha.

Ukweli ni kwamba, ule usemi usemao hasira hasara, haujakosea hata kidogo, endapo mtu atashindwa kudhibiti hasira zake akiwa na mwenza wake, kuna hatari ya kufanya mambo mabaya ambayo baadaye baada ya hasira kushuka kujikuta anajuta.

Ingawa ni kweli si rahisi nyakati zote kudhibiti hisia zako, lakini unaweza kudhibiti maneno na matendo yako. Hakuna haja ya kulipuka kwa hasira pindi mwenza wako anapokosea au inapotokea tofauti kati yenu.

Facebook Comments