Mzee aliyechora Nembo ya Taifa afa na ndoto yake

MZEE Francis Kanyasu maarufu kama Ngosha (86) ambaye amefahamika hivi karibuni kuwa ndiye aliyebuni Nembo ya Taifa (yenye alama ya bibi na bwana) amefariki Dar es Salaam jana.

Mzee huyo alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amehamishiwa kwa matibabu, siku mbili tu baada ya Rais John Magufuli na mkewe, Janeth, kumjulia hali hospitalini hapo.

Amefariki kabla hajatimiza azma yake ya kuchora na kukabidhi kwa Rais John Magufuli, picha yake pamoja na picha nyingine alizoahidi kuzichora alipotembelewa na Rais huyo mwishoni mwa wiki. Jana Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kufariki kwa mzee huyo ikisema kuwa alifikwa na umauti juzi usiku saa mbili wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Mzee huyo mkazi wa Buguruni mtaa wa Malapa, alihamishiwa hospitali ya Muhimbili akitokea Hospitali ya Rufaa ya mkoa Amana alikolazwa baada ya kupelekwa na wasamaria wema wiki iliyopita. Baada ya kufanyiwa vipimo na kuanzishiwa tiba Amana na habari zake kutangazwa na vyombo vya habari, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Dk Khamis Kigwangala aliingilia kati na kuagizwa ahamishiwe Muhimbili.

Alipotembelewa na Rais alikuwa anaendelea vyema. Mwandishi wa habari wa gazeti hili jana alifika Buguruni Mtaa wa Malapa, Nyumba Namba 32 jijini Dar es Salaam ambako ndiko alipokuwa akiishi Mzee Ngosha kabla ya umauti kumkuta na kukuta wanafamilia wa nyumba ya marehemu Mzee Yusuph Salum maarufu kama Digogogo wakiomboleza.

Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa wanafamilia, Said Chume alisema Mei 27, mwaka huu Mzee Ngosha akiwa Hospitali ya Muhimbili amelazwa, aliwaeleza apelekewe hospitali hapo brashi na rangi ili amchore Rais Magufuli, marais wastaafu Jakaya Kikwete na Mwalimu Julius Nyerere.

Rais Magufuli alifika Hospitali ya Muhimbili, Jumapili kuwajulia hali wagonjwa mbalimbali waliolazwa wodi ya Mwaisela akiwemo Mzee Ngosha na mtoto mwenye matatizo ya lishe aliyekuwa akila mafuta.

“Alitusisitiza tumpelekee vitu hivyo ili aweze kuchora picha hizo ili amkabidhi Rais Magufuli kama zawadi na picha nyingine alituambia kuwa ameshazichora,” alisema Chume akimkariri mzee huyo.

Chume alisema, Mzee Ngosha alikuwa na furaha kubwa kwamba sasa hata akifa ametambuliwa na viongozi wa serikali kwamba ana mchango wake katika taifa kupitia picha ya nembo aliyochora.

“Hata kama amekufa atakuwa ana furaha kubwa, alikuwa anasema ujumbe wake umefika kuwa ametoa mchango katika taifa na amefahamika kwa umma na serikali,” aliongeza mtu huyo.

Kabla ya kufariki, mzee huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye ndiye aliyebuni nembo ya Taifa baada ya kuombwa na Mwalimu Julius Nyerere miaka ya 60 kabla ya uhuru akifanya kazi mashamba ya mkonge Tanga.

Madai hayo yalithibitishwa na mjane wa mwenzake aliyekuwa naye. Akimzungumzia mzee huyo kuwa hana ndugu kama vyombo vya habari vilivyoripoti, Yusuph Salum ambaye ni mjukuu wa marehemu Mzee Yusuph aliyempokea alisema anaamini Ngosha ni ndugu yao.

“Kusema mzee huyu hana ndugu ni kosa, nyumba hii tunaishi kama familia moja na sisi ni wajukuu zake. Mzee alipokelewa na babu yangu mwaka 1991 na tumeishi naye miaka yote kama ndugu yetu mpaka umauti wake,” alifafanua Salum.

Alisema anasikitika kuwa mzee huyo amefariki, lakini hawajapewa taarifa yoyote kutoka hospitali badala yake wanapigiwa simu na vyombo vya habari na kusikia taarifa kupitia redio zikidai amefariki. “Kama wanadai mzee hakuwa na ndugu, siku zote alikuwa anaishi wapi?

Tumemlea kama babu yetu na sisi ametulea sana akiwa kijana,” aliongeza kijana huyo. Yusuph ambaye anamwita Mzee Ngosha babu, alisema mzee huyo alifika kwenye nyumba hiyo kama mpangaji, lakini hakuweza kulipa kodi na waliendelea kuishi naye kama ndugu na kwamba hawakuwahi kuona ndugu yake mwingine yeyote.

Akimzungumzia maisha yake, alisema alikuwa ni mtu mkarimu anayependa watu na kwamba alikuwa akichora picha zake mpaka anapelekwa hospitali baada ya kuzidiwa na maradhi aliyokuwa nayo. Mjumbe wa mtaa huo, Jumanne Milandu alisema mzee huyo alikuwa mkarimu na kipenzi cha watu.

“Hakuwahi kugombana na mtu, alikuwa akizunguka na makopo yake ya rangi akichora picha mitaani, hata akiletwa kuzikwa huku watu watajaa kwa upendo waliokuwa nao juu yake,” alieleza.

Kwa nyakati tofauti, mzee huyo alizungumziwa kuwa mchoraji wa picha mbalimbali hasa za kitalii alizoziuza na fedha hiyo kuishia katika chakula na mavazi. Wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla alipomtembelea Hospitali ya Amana, alisema serikali itasaidia matibabu ya mzee huyo ikiwa ni wajibu wake kwa kuthamini mchango wa wasanii lakini zaidi kwa kuchora kwake nembo. Haikufahamika mara moja kama serikali ina mpango wowote kusimamia mazishi ya mzee huyo.

Facebook Comments