Aisafiria ‘Ndondo Cup’ kutoka Musoma hadi Dar

Nembo rasmi ya michuano ya Ndondo Cup

Kijana Magela Peter amelazimika kupanda basi na kusafiri kutoka Musoma mkoani Mara hadi Jijini Dar es Salaam kusaka nafasi ya kushiriki michuano ya ‘Ndodo Cup’ inayoanza kutimua vumbi lake Jumamosi ya Juni 17 na kurushwa moja kwa moja na Azam TV

Kijana huyo mwenye kipaji cha kusakata kabumbu, anaamini kuwa endapo atapata nafasi katika michuano hiyo, itakuwa ni fursa muhimu kwake kujitangaza na kuonekana kwa vilabu vikubwa, hatua itakayomfungulia njia katika maisha yake ya soka.

“Ndondo Cup ni pana sana na inatoa fursa kubwa kwa vijana wengi kuonekana, na pia ikuwa ni fursa kwangu kuonesha uwezo wangu”

Akizungumza na waratibu wa michuano hiyo ambao ni Clouds Media, Peter amesema amekuwa akiifuatilia michuano hiyo ambayo tangu ianze imekuwa ikifanyikia Dar es Salaam, lakini alivutiwa zaidi pale ilipoanza kuoneshwa kwenye TV kupitia chaneli za azam TV.

“Nimekuwa nikiisikia lakini mwaka jana walipoanza kurusha kwenye TV ndiyo nikavutiwa zaidi na kilichokuwa kinanifanya nisije mapema ni shule maana nilikuwa ndo namaliza form four, na sasa nilikuwa nasubiri nimalize mitihani yangu ya kidato cha sita ambayo nimemaliza mwezi wa tano” Amesema Peter.

Akizungumzia timu anayoikubali zaidi katika michuano hiyo, Peter mwenye uwezo wa kucheza kama mlinzi wa kati au kiungo ameitaja kauzu FC kuwa ndiyo timu anayotamani kuichezea, ingawa yuko tayari kujiunga na timu yoyote kati ya timu 32 zinazoshiriki mashindano hayo.

Akizungumzia uzoefu wake wa kusakata kabumbu, kijana huyo amesema amewahi kukipiga katika ligi daraja la pili akiwa na Bulyanhulu ya Shinyanga, lakini pia amecheza sana katika michuano ya Ester Bulaya Cup iliyokuwa chini ya Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya

Amewaasa vijana wenzake wenye malengo ya kucheza mpira katika kiwango cha juu kuwa na nidhamu, kujituma katika mazoezi na kujitambua

CHANZO AZAM TV

Facebook Comments