Mwakyembe aridhishwa na ukarabati wa Uwanja wa Taifa

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akionyeshwa mashine zinazotumika katika ukarabati wa picth katika uwanja wa Taifa kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.Alex Nkenyenge . katikati ni Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw. Julius Mgaya na kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji kutoka SPORTPESA Bw.Tarimba Abbas leo Jijini Dar es Salaam .

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe ameridhishwa na maendeleo ya ukarabati wa eneo la kuchezea mpira (picth) la Uwanja wa Taifa wakati wa ziara yake leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe(mwenye miwani) akisikiliza maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Alex Nkenyenge (wa Tatu kulia) alipotembelea uwanja wa Taifa leo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika ziara hiyo ya kukagua hatua iliyofikiwa katika matengenezo ya uwanja huo Waziri Mhe.Dkt. Mwakyembe amesema kuwa amefurahishwa na hatua ya awali ya ukarabati na anatarajia mabadiliko makubwa zaidi baada ya hatua zinazofuata kukamilika .

“Nimefurahishwa na mabadiliko niliyoyaona katika hatua hii ya awali naamini ukarabati utakapokamilika milango itakuwa wazi kwa mechi za kimataifa ikiwemo mashindano ya AFCON yanayoratajiwa kufanyika nchini kwetu mwaka 2019” alisema Dkt.Mwakyembe

Aidha aliongeza kwa kusema kuwa Serikali ipo katika mkakati wa kuhakikisha viwanja vingine vikiwemo vya mikoani vinafanyiwa ukarabati ili kuboresha sekta ya michezo nchini.

Waziri Dkt. Mwakyembe ameushukuru uongozi wa SPORTPESA kwa kuonyesha ushirikiano wa karibu na Serikali katika kuhakikisha inaweka mchango wake katika michezo kwa kukarabati sehemu ya kuchezea mpira (picth) ya Uwanja wa Taifa pamoja na vifaa mbalimbali vilivyotolewa katika kuhakikisha kazi hiyo inakamilika.

Naye Mkurugenzi wa Utawala Na Utekelezaji kutoka SPORTPESA Bw.Tarimba Abbas ameeleza kuwa kampuni yao imefanya hivyo ikiwa ni njia ya kuonyesha uzalendo wa kupenda na kuthamini vya nyumbani.

“Hatua hii ni ya awali baada ya mechi ya Everton na Gorimahiya mnamo Julai 13 mwaka huu hatua itakayofuata ni ya kuondoa nyasi zote na kuotesha mpya ambazo zitachukuwa miezi mitatu kuwa sawa” alisema Bw.Tarimba.

Uwanja wa Taifa ulianza matengenezo ya eneo la kucheze (pitch) rasmi katikati wa mwezi wa sita lengo ni kuhakikisha nyasi zilizochakaa zinaondolewa na kuwekwa nyasi mpya zitazodumu zaidi ya miaka 10 .

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akielezwa jambo kuhusu matumizi mashine ya kuchorea mistari kutoka kwa Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw. Julius Mgaya(aliyeinama) na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.Alex Nkenyenge leo Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kutembelea uwanja huo.
Facebook Comments