Auawa akimuokoa mdogo wake asibakwe

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Innocent Lameck (22) mkazi wa Mtaa wa Nyanshana wilayani Nyamagana, kwa tuhuma za mauaji ya kijana aitwaye Sangija George (27) yaliyotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni.

Kamanda wa Jeshi hilo, DCP Ahmed Msangi, amesema tukio hilo limetokea Juni 25, 2017 saa 5 usiku wakati marehemu alipokwenda kumuokoa mdogo wake asibakwe na mtuhumiwa pindi alipokwenda kujisaidia chooni.

Inadiwa kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo alikuwa amepewa hifadhi ya malazi ya muda nyumbani kwao marehemu kwa kuwa sehemu alipokuwa amefikia hapakuwa na nafasi.

Kamanda Msangi amesema kuwa siku ya tukio mdogo wa marehemu ambaye ni wa kike mwenye umri wa miaka 12, mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Nyashana alikwenda chooni kujisaidia ndipo mtuhumiwa alimfuata chooni na kuanza kumbaka.

“Inasemekana kuwa wakati mtuhumiwa wa mauaji hayo anatekeleza tukio la ubakaji huko chooni binti alipiga yowe kuomba msaada, marehemu aliposikia alikwenda chooni kumuokoa mdogo wake ndipo alichomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mtuhumiwa kinachodaiwa kuwa ni kisu na kufariki dunia njiani wakati akikimbizwa hospitali,” amesema Kamanda Msangi.

Amesema jeshi hilo linaendelea na mahojiana na mtuhumiwa, pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Facebook Comments