Kamanda wa polisi achaguliwa kuwa mwenyekiti CCM

Aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
(SACP), Absolom Mwakyoma amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
katika Kata ya Mfumuni, Manispaa ya Moshi baada ya kupita bila kupingwa.

Mwakyoma ambaye pia amewahuku kuwa Kamanda wa Polisi katika mikoa ya Pwani na Mara
kwa nyakati tofauti, alishinda kiti hicho baada ya kukosa mpinzani na hivyo wajumbe wote 25
waliokuwepo kumpigia kura ya Ndiyo.

Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa CCM Manispaa ya Moshi, Sixtus Mosha alisema kuwa
Mwakyomba alichukua fomu mwenyewe bila kupingwa na hivyo kumuwezesha kupata ushindi
huo mkubwa.

“Mwakyoma alijitokeza peke yake kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo Agosti 3 na kisha akachaguliwa kwa kupita bila kupingwa Agosti 6, mwaka huu.”

Hakuna namna nyingine zaidi ya kuwapa ushirikiano wa kukijenga chama chetu hawa viongozi waliochaguliwa, na siyo kujenga makundi au majungu. Tunataka wawe mstari wa mbele kumuunga mkono Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli kutekeleza ilani sawa sawa,” amesema Sixtus.

Viongozi wa CCM katika manispaa hiyo waliwataka wanachama wao kuhakikisha wanawachagu wagombea wa CCM ili, kwanza, waendane na kasi ya Rais Dkt Magufuli, lakini pili, kurahisisha ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Mwakyoma alikuwa RPC wa Mkoa wa Kilimanjaro, kati ya mwaka 2011 hadi 2012 akichukua nafasi ya Lukas Ng’hoboko aliyekuwa mtangulizi wake katika kiti hicho kati ya mwaka 2006 hadi 2011.

Baadae, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wakati huo, Said Mwema akafanya mabadiliko na RPC Kilimanjaro, SACP Absalom Mwakyoma ambaye akahamishiwa mkoani Mara akibadilishana na RPC Mara, ACP Robert Boaz ambaye alihamishiwa mkoa wa Kilimanjaro.

Facebook Comments