Niyonzima aahidi zawadi kwa Kazimoto

Nyota mpya wa Simba aliyesajiliwa hivi karibuni baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga, Haruna Niyonzima ameahidi kumtafutia zawadi kiungo mkongwe wa klabu hiyo, Mwinyi Kazimoto kutokana na hatua yake ya ‘kumvulia jezi.

Kazimoto aliyekuwa akivaa jezi namba 8, ameamua kumuachia kiungo huyo raia wa Rwanda baada ya kuombwa kufanya hivyo kama ishara ya heshima kwake.

“Namshukuru sana Mwinyi kwa heshima aliyonipa, na mimi namuahidi kumtafutia zawadi, ni lazima nimzawadie kwa hili alilonifanyia” amesema Haruna

Akizungumzia sababu za kuiomba jezi hiyo, Haruna ambaye mara nyingi hucheza kama kiungo namba 8, amesema jezi hiyo ina kumbukumbu kubwa katika maisha yake ya soka, na ndiyo aliyokuwa akiivaa wakati akiwa Yanga

Niyonzima ambaye ameanza kuonyesha cheche katika klabu ya Simba kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports iliyopigwa jana kuadhimisha Simba Day, ameahidi kuitumikia Simba kwa nguvu zote katika mechi zote na amesema ataanza na mechi ijayo ya ‘Ngao ya Jamii’ dhidi ya timu yake ya zamani, Yanga.

“Kama ikitokea nikaifunga Yanga, nitashangilia lakini kwa heshima kwa sababu wale ni kama ndugu zangu,” alisema Niyonzima.

Kuanzia sasa Mwinyi Kazimoto atakuwa akivaa jezi namba 24 ambayo ilikuwa haina mtu na Emmanuel Okwi aliyeng’ara klabuni hapo miaka ya nyuma akiwa na jezi namba 25, sasa atavaa jezi namba 7 na kuiacha jezi hiyo kwa Shiza Kichuya.

Facebook Comments