Utoaji maeneo mapya ya utawala, wasitishwa

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imesitisha zoezi la kutoa maeneo mapya ya utawala hadi itakapotangazwa vinginevyo.

“Kwa sasa tumesitisha kutoa maeneo mapya ya utawala ili tuimarishe kwanza yale ya awali. Tunaimarisha kwanza miundombinu ya majengo ya ofisi, nyumba za watumishi kwenye wilaya na halmashauri mpya, zikitengamaa tutafanya maamuzi mapya, ” amesema.

Waziri mkuu ametoa kauli hiyo Ulyankulu wilayani Kaliua mkoani Tabora wakati akijibu maombi ya wabunge wa majimbo ya Ulyankulu na Kaliua ambao walisema kuna haja ya kuigawa wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye kata zilizo mbali na tarafa.

Akizungumzia kuhusu migogoro baina ya wanavijiji na maeneo ya hifadhi, waziri mkuu amesema serikali bado inafanya uhakiki wa mipaka katika maeneo ya hifadhi na ikikamilisha zoezi hilo itatoa taarifa.

Ili kuharakisha zoezi hilo, waziri mkuu amewataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi, wasifanye upanuzi wowote hadi zoezi la kuhakiki mipaka ya hifadhi litakapokamilika.

“Tumeamua kuweka beacons katika maeneo yote ya hifadhi ili kubaini mipaka imepita wapi. Wananchi mkiwaona watu wa hifadhi wanapita huko msigombane nao. Ni hatua ya awali ya kubaini maeneo ya mipaka. “

Facebook Comments