Yanga yahaha kulinusuru jengo lake

Uongozi wa klabu ya Yanga umeeleza kushtushwa na hatua ya serikali kutaka kulipiga mnada jengo la makao ya klabu hiyo lililopo mtaa wa Jangwani Jijini Dar es Salaam kutokana na kukabiliwa na kodi ya ardhi.

Katibu mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amekiri Yanga kudaiwa kodi hiyo, huku akisita kutaja kiasi halisi inachodaiwa

Mkwasa amewataka wapenzi wa soka nchini hususani wana Yanga kuwa watulivu kwa kuwa uongozi wa klabu unalifanyia kazi na kwamba utatoa taarifa rasmi baadaye

“Ni kweli tuna deni kubwa tunadaiwa la ardhi, lakini tayari tulifanya nao mazungumzo na kukubaliana namna ya kulilipa kupitia mapato yetu ya milangoni. Tatizo ni kwamba hapa katikati ligi ilisimama, lakini hivi karibuni inaanza na tutaendelea kulipa, Tutatoa taarifa rasmi baadaye”. Amesema Mkwasa

Mkwasa amesema kiasi wanachodaiwa ni kikubwa lakini hakizi shilingi milioni 500, huku akiweka wazi kuwa pesa wanayotakiwa kulipa kwa mwaka ni shilingi milioni 59.

Wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi kupitia kwa kampuni ya udalali ya Msolopa Investmenst Limited leo imetangaza kulipiga mnada jengo hilo endapo Yanga hawatalipa kabla ya Agosti 19, mwaka huu.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*