Kocha wa simba hana muda atatimuliwa:Edo kumwemba

HAITAPITA muda mrefu, kocha anayeitwa Joseph Omog anaweza kunipigia simu nimpeleke Uwanja wa Ndege kwa safari ya kurudi kwao Cameroon. Muda si mrefu tiketi yake ya kuelekea katika Uwanja wa Ndege wa Younde inaweza kuwa tayari.

Zimeanza kelele baada ya kikosi cha Sh1.3 bilioni cha Simba kutoka suluhu ya bila kufungana na Mlandege paleZanzibar usiku wa Alhamisi. Haijalishi kama atashinda pambano dhidi ya Yanga, Omog hana maisha marefu sana Msimbazi.

Nimekutana na vikundi vya Wanamsimbazi ambao wanamsema vibaya kocha wao. Katika soka letu ukiona watu wameanza vikundi vikundi wakisifu viongozi zaidi kwa usajili uliofanywa huku wakiguna kuhusu matokeo, basi ujue hapo safari ya kocha imewadia.

Kuna sababu mbili. Sababu ya kwanza ipo duniani kote. Jinsi timu inavyotumia pesa nyingi ndivyo makocha wanavyowekwa katika presha. Waulize makocha waliopita, Chelsea, Manchester City, Real Madrid na PSG watakavyokwambia.

Ni kitu cha kawaida. Matumizi ya pesa yanasababisha kitu kinachoitwa BRN yaani Big Results Now. Au kwa Kiswahilini Matokeo ya Haraka haraka sasa hivi. Bahati mbaya zaidi kwa Omog bado hata hajaifanyia timu makubwa.

Kuna makocha ambao waliwahi kuzipa ubingwa wa LigiKuu timu zao, katika ligi ngumu kama vile Roberto Mancini, Manuel Pellegrini, Jose Mourinho lakini waliishiwa kufukuzwa msimu mmoja tu baada ya kuwa mabingwa. Itakuwa kwa Omog ambaye amewapa Kombe la FA tu?

Hiki ndicho kinachomkabili Omog. Sababu za kisoka zinamezwa na matumizi ya pesa na uwezo wa mastaa walionunuliwa kama kina Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, John Bocco na wengineo uwanjani.

Hakuna ambacho Omog anaweza kujitetea kwa sasa. Amewekwa katika presha. Sababu ya pili ni nje ya sababu za kawaida za kisoka huko duniani. Hii ni sababu yetu binafsi katika soka la Tanzania. Tuna vigezo tofauti vya kufukuza makocha.

Ulaya ni nadra kwa kocha kufukuzwa wakati wa maandalizi ya msimu. Kocha huwa anaondolewa wakati
msimu unaendelea au wakati msimu unapoisha. Hapa kwetu kocha anaweza kuondolewa wakati wowote ule kwa madai kwamba kiwango chake kipo chini dhidi ya viwango vya mastaa wapya walionunuliwa.

Kuna hesabu ambazo kwa kawaida kocha anaweza kuzipiga kabla ya msimu kuanza. Analazimika kujaribu kombinesheni tofauti baada ya kuletewa rundo la wachezaji 14 wapya. Hata hivyo, hatavumiliwa kwa sababu wachezaji wenyewe ni mastaa zaidi.

Tusubiri, inawezekana Omog hajapata kikosi chake cha kwanza anachokihitaji.

 

Facebook Comments