Yanga yatoa tamko kuondoka Lwandamina

Taarifa iliyotolewa na Yanga ikiambatana na tiketi inayosambaa mitandaoni

Klabu ya Yanga imekanusha taarifa za kocha wake mkuu Mzambia, George Lwandamina kuwa yuko mbioni kuachana na timu hiyo na kurejea nchini kwao Zambia.

Taarifa ya Yanga inakuja baada ya kuenea kwa nakala ya tiketi ya kocha huyo ikionesha kuwa kesho majira ya saa nne usiku Lwandamina ataondoka jijini Dar es Salaam kurejea Lusaka.

Uongozi wa Yanga kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram umeandika kuwa taarifa hizo ni za uongo na kuwataka wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo kuzipuuza.

Katika hatua nyingine klabu ya Yanga kesho majira ya saa tano kamili asubuhi itakuwa na mkutano na wafanyabiashara, waigizaji na wauzaji wa vifaa mbalimbali vya michezo vyenye nembo ya Yanga nchini.

Baada ya mkutano huo Yanga imetangaza kuwa haitakuwa na msamaha kwa wauzaji holela na magendo wa vifaa vyenye nembo ya klabu hiyo.

Facebook Comments