Martin aziba pengo la Msuva, Stars

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amemwongeza kiugo wa Yanga, Emmanuel Martin kwenye kikosi chake kinachojiandaa kucheza na Botswana Jumamosi Septemba 2, mwaka huu.

Kiungo huyo ambaye ameonekana kujituma katika michezo kadhaa ya kikosi cha Yanga, ameongezwa na Mayanga baada ya mawasiliano kuonesha kwamba huenda akawakosa nyota wa kimataifa Simon Msuva kutoka Difaa El Jadidah ya Morocco na Orgenes Mollel wa FC Famalicao ya Ureno.

Taarifa kutoka Morocco inaonesha kwamba Msuva ana kibali cha muda cha kuingia na kutoka Morocco ‘visa’ ambacho kinamnyima haki ya kutoka na kuingia Morocco mara kwa mara.

Martin amejiunga na kambi ya Taifa Stars leo Agosti 30, mwaka huu na kuendelea na mazoezi na wenzake kwenye uwanja huo wa Uhuru.

Nyota wengine wote wameripoti Taifa Stars wakiwamo wale wa kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kama vile Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Elias Maguli (Dhofar FC/Oman), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya) wakati Farid Mussa wa CD Tenerif ya Hispania akitarajiwa kutua leo.

Wengine ambao wako kambini ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).

Pia wamo Walinzi Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).

Viungo ni Himid Mao – Nahodha Msaidizi (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Shiza Kichuya (Simba SC), wakati Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans) na Kelvin Sabato (Azam FC).

Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam chini ya utaratibu wa kalenda ya FIFA utarushwa mbashara kupitia Azam TV

Facebook Comments