Mwanafunzi kidato cha 4 ajifungua Darasani.

Mwanafunzi wa kidato cha nne aliyejulikana kwa jina la Amina Kanju mwenye umri wa miaka 19 katika shule ya sekondari Mbelei iliyopo Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga, amejifungua katika mazingira ya shule wakati alipokuwa kwenye mitihani ya maandalizi ya kidato cha nne kwa mwaka 2017.

Tukio hilo limetokea Agosti 29 mwaka huu majira ya saa nane mchana wakati mwanafunzi huyo akiwa anaendelea na mitihani hiyo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Abnaigwa Bakuki amesema kuwa mwanafunzi huyo ambaye alikuwa na tabia ya utoro alifika shuleni hapo siku ya mtihani na kuingia darasani lakini wakati alipokuwa akiendelea na mitihani hiyo gafla alianza kuumwa.

Mwalimu mkuu huyo amesema kuwa hakuna mtu yeyote shuleni hapo aliyekuwa akitambua juu ya ujauzito wa mwanafunzi huyo kutokana na tabia ya utoro.

Shule hiyo haina mabweni ya kutosha jambo ambalo linasababisha baadhi ya wanafunzi kukaa manyumbani mwao huku wengine wakiwa wamepanga nyumba.

Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya ya Lushoto January Lugangika ametoa onyo kwa walimu walioko kwenye mazoezi ya kufundisha kutojishirikisha katika mapenzi na wanafunzi.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa ili kuhakikisha wanakomesha vitendo kama hivyo katika wilaya hiyo atahakikisha kila shule inakuwa na mabweni ya kutosha.

Facebook Comments