Simba kumburuta Buswita mahakamani

Suala la kiungo wa zamani wa Mbao FC ya Mwanza Pius Buswita kufungiwa kwa mwaka mmoja kucheza mpira wa miguu limechukua sura mpya baada ya klabu ya Simba kuamua kumpeleka mahakamani mchezaji huyo kudai kurejeshewa fedha zake.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari, uongozi wa Simba umesema umeamua kuchukua uamuzi huo baada ya Pius Buswita kutoa kauli za uongo dhidi ya viongozi hao.

Simba imesema inaenda mahakamani kwa lengo moja kubwa la kutaka vyombo vya sheria vichukue hatua stahiki pamoja na klabu hiyo kurejeshewa fedha za usajili walizomlipa kabla ya kuamua kusaini Yanga.

Juma lililopita kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji ya shirikisho la soka nchini TFF, ilitangaza kumfungia Pius Buswita kwa kile kinachoelezwa kuwa alivunja moja ya kanuni za ligi kuu ya Tanzania bara.

Pius Buswita amethibitika kuwa alisaini katika klabu ya Simba kabla ya kusaini tena kwa watani wao wa jadi Yanga, kosa la kikanuni lililomtia hatiani kiasi cha kufungiwa kwa mwaka huu.

Baada ya adhabu hiyo Pius Buswita alinukunuliwa katika moja ya vyombo vya habari nchini kuwa alitolewa vitisho yeye pamoja na mama yake mzazi kabla ya kulazimishwa kusaini mkataba huo na klabu ya Simba.

Facebook Comments