Azam yauzima moto wa Simba

Moto iliyoanza nao klabu ya Simba kwenye ligi kuu Tanzania Bara msimu huu wa kuishushia Ruvu Shooting kipigo cha mabao 7-0 katika dimba la Uhuru, umezimwa hii leo katika dimba la Azam Complex, Chamazi.

Waliohusika kuuzima moto huo ni vijana wanaounda kikosi cha mabingwa wa Afrika Mashariki na kati Azam FC kwa kuwalazimisha vijana hao wa Msimbazi suluhu ya bila kufungana katika mchezo wa raundi ya pili.

Katika mchezo huo uliorushwa moja kwa moja kupitia channel ya Azam Sports 2, kumeshuhudiwa upinzani wa hali wenye kukamiana, huku kukiwa na kosakosa za kusisimua kwa pande zote mbili.

Simba ikiwa na wachezaji watatu waliokuwa Azam msimu uliopita ambao kipa Aishi Manula, Erasto Nyoni na John Bocco imewakosa Juuko Murshid na Emmanuel Okwi wakati Azam ikiwa na muziki wake kamili kikiongozwa na beki Yakub Mohamed ambaye kwa kiasi kikubwa amefanikiwa kuidhibiti safu ya ushambuliaji ya Simba akishirikiana na Agrey Morris.

Kwa matokeo haya, Simba ambayo imecheza mchezo wake wa kwanza wa kimashindano katika dimba la Chamazi, imefikisha point 4 ikiwa nafasi ya kwanza mbele ya Azam FC ambayo pia ina point 4.

Facebook Comments