Uchambuzi wa awali Manchester City Vs Liverpool

Manchester City na Liverpool wataingia dimbani Etihad mapema Jumamosi katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Uingereza

Timu zote mbili zimo ndani ya nne bora za kwenye msimamo wa Ligi zikiwa zimejikusanyia alama saba kutoka kwenye mechi zao tatu za mwanzo, ingawa City bado hawajashinda mechi ya nyumbani kwani walilazimishwa sare ya 1-1 na Everton.

Kwa upande wa Liverpool, wameshinda mechi zote za nyumbani – ikiwa ni pamoja na kipigo cha 4-0 walichoipa Arsenal – lakini walipata sare pekee ya 3-3 dhidi ya Watford mechi ya ufunguzi.

Ushindi kwa aidha Guardiola au Klopp Jumamosi utampandisha mshindi yeyote kileleni – angalau kabla ya Manchester United kucheza baadaye siku hiyo, hata hivyo hakuna meneja anayetamani kufungwa kuipa Man United fursa ya kujiimarisha kileleni.

Man City watakuwa wenyeji wa Liverpool katika uwanja wa Etihad, Septemba 9, na mechi inatarajiwa kuanza saa nane za mchana kwa saa za Afrika Mashariki.

Kuna uwezekano mkubwa Alex Oxlade-Chamberlain ataanza beki ya kulia kwa Liverpool baada ya kuthibitika kuwa Nathaniel Clyne anasumbuliwa na majeraha ya mgongo.

Lakini pia haijaeleweka kama Philippe Coutinho atacheza mechi hiyo muhimu baada ya kukosekana dimbani muda mrefu huku mipango yake ya kujiunga na Barcelona ikigonga mwamba.
Ubashiri wa Kikosi:

Man City XI: Ederson, Walker, Kompany, Otamendi, Mendy, De Bruyne, Fernandinho, Silva, Bernardo Silva, Jesus, Sterling

Liverpool XI: Mignolet, Oxlade-Chamberlain, Matip, Lovren, Moreno, Can, Henderson, Wijnaldum, Salah, Firmino, Mane

Facebook Comments