‘Media Center’ ya kisasa yazinduliwa Azam Complex

Klabu ya Azam FC imezindua chumba maalum cha kufanyia mikutano ya waandishi habari (Media Center) chenye hadhi ya kimataifa kilichopo kwenye makao makuu ya timu hiyo Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Zoezi hilo limeongozwa na mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Abdul Mohamed, mara baada ya mchezo wa ligi kuu Tanzania kati ya Azam FC na Simba SC uliopigwa kwa mara ya kwanza katika uwanja huo.

Zoezi hilo limehudhuriwa pia na mkuu wa kItengo cha habari na mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas pamoja na yule wa Simba, Haji Manara, ambao waliipongeza timu hiyo kwa kuzidi kufanya mapinduzi kwenye soka la Tanzania.

Kwa upande wake Lucas, amesema hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya fainali ya AFCON kwa vijana mwaka 2019, ambazo zitaandaliwa nchini Tanzania, na uwanja huo ni moja ya viwanja vitakavyotumika.

Chumba hicho cha habari kina hadhi ya kimataifa, kwa Afrika Mashariki na Kati kikiwa kinashika nambari moja kikisheheni kila kitu kwa ajili ya kufanikisha mikutano pamoja na kazi za waandishi wa habari.

Miongoni mwa huduma zilizomo katika kituo hicho ni pamoja na intaneti ya bure (Free Wifi) kwa waandishi wa habari ili kuwawezesha kufanya kazi zao na kuzituma kwenye vyombo vyao vya habari kwa haraka na urahisi.

Pia kuna televisheni maalum ambayo itakuwa ni kwa ajili ya wanahabari ambao wanaweza kuwa wakifuatilia mechi inayoendelea uwanjani hapo huku wakifanya kazi zao.

Abdul Mohamed amesema mbali na kituo hicho, pia panaandaliwa mahali kwa ajili ya makumbusho ya klabu ambayo mtu yeyote akifika hapo ataweza kupata historia kamili ya klabu hiyo pamoja na kuona vitu mbalimbali ambavyo vimewahi kutumiwa na klabu hiyo.

Facebook Comments