Yanga Yaonja ladha ya ushindi wa kwanza mbele ya Njombe Mji

Mshambuliaji wa Yanga aliyechomolewa kutoka kwa mahasimu wao, Simba SC, Ibrahim Ajibu Migomba, amefungua rasmi kitabu chake cha mabao kwa kuifungia Yanga bao pekee na la ushindi dhidi ya Njombe Mji.

Mchezo huo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa katika dimba la Sabasaba mjini Njombe, umeshuhudia Yanga ikiondoka na ushindi wa bao 1-0 na hivyo kubeba pointi zote tatu ugenini.

TAZAMA BAO WALILOLIPATA YANGA HAPO CHINI

Yanga ambao ndiyo mabingwa watetezi wa ligi hiyo, walianza mchezo huo kwa mashambulizi ya kasi, yaliyopelekea wenyeji Njombe Mji kupoteana na kujikuta wakicheza rafu za mara kwa mara.

Moja kati ya rafu waliyocheza wenyeji hao ndiyo iliyozaa bao kwa ‘free kick’ ya kiufundi wa hali ya juu iliyopigwa na Ibrahim Ajibu katika dakika ya 16 ya mchezo, bao lililodumu hadi dakika ya 90 licha ya Njombe kuzinduka katika dakika za mwisho.

Kwa takriban dakika 30 za mwisho Yanga walionekana ‘kupaki basi’ na kuruhusu mashambulizi kutoka kwa Njombe Mji, lakini hata hivyo mashambulizi hayo hayakubadilisha kitu kwani kipa wa Yanga Youthe Rostand alisimama imara na kuokoa michomo takriban mitatu kutoka kwa Njombe.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 4 na kukwea hadi nafasi ya tano baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lipuli FC katika mchezo wa kwanza, huku Mji Njombe ikiwa nafasi moja kutoka mkiani, nafasi ya 15 ikiwa haina pointi hata moja kutokana na kupoteza michezo yote miwili ya kwanza.

Katika michezo mingine iliyopigwa leo, Mtibwa Sugar iliyokuwa Manungu Morogoro imeichapa Mwadui FC bao 1-0, Singida United imeichapa Mbao FC mabao 2-1 katika dimba la Jamhuri Dodoma, Lipuli FC iliyokuwa nyumbani imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand united.

Katika dimba la Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting wakati Mbeya City ikichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka Ndanda FC, dimba la Sokoine.

Facebook Comments