Mtibwa Sugar yatamba kileleni VPL

Mtibwa Sugar kutoka Manungu Morogoro, imekalia usukani wa ligi kuu Tanzania Bara baada ya kushinda mchezo wake wa pili mfululizo na kufikisha jumla ya pointi 6.

Mtibwa inakuwa ndiyo timu pekee iliyoshinda mechi zote mbili mfululizo, baada ya kukamilika kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo ambapo jana kiliipiga Mwadui FC bao 1-0 katika uwanja wa Manungu Turiani Morogoro na kunasa pointi zake 3, wakati katika mchezo wa kwanza iliifunga Stand United bao 1-0.

Licha ya wadau na wachambuzi wa soka kuitabiria mabaya timu hiyo wakitumia historia yake ya kufanya vizuri mwanzoni mwa ligi huku ikiharibu mwishoni, Mtibwa wao wametamba kuendelea na moto huo hadi mwisho wa msimu.

Msimamo wa ligi hiyo hadi sasa ambapo kila timu imecheza mechi mbili unaonesha kuna timu tano zenye point 4 kila moja ambazo ni Simba ikiwa nafasi ya pili, Tanzania Prisons nafasi ya tatu, Lipuli FC nafasi ya nne, Yanga iliyo nafasi ya tano na Azam FC ikiwa nafasi ya sita. Timu hizi zimeshinda mechi moja na kutoka sare mechi moja.

Timu zenye point tatu kila moja ziko tano ambazo ni pamoja na Singida United nafasi ya saba, Mbao FC nafasi ya nane, Mwadui Fc nafasi ya tisa, Mbeya City nafasi ya kumi na Ndanda FC ambayo jana imeipiga Mbeya City 1-0, ikishika nafasi ya 11. Timu hizi zimeshinda mechi moja na kufungwa mechi moja.

Timu tatu bado zina point moja zikiwa zimetoka sare mchezo mmoja na kufungwa mchezo mmoja zikiongozwa na Majimaji FC iliyo nafasi ya 12, Kagera Sugar nafasi ya 13 na Ruvu Shooting nafasi ya 14.

Hadi sasa kuna timu mbili ambazo hazina pointi hata moja, zikiwa zimepoteza michezo yake yote miwili ya kwanza. Timu hizo ni Njombe Mji iliyofungwa jana na Yanga, ikikamata nafasi ya 15 pamoja na Stand United ambayo msimu huu imeanzia mechi zake zote mbili ugenini na kuchezea vichapo katika mechi zote.

Stand ambayo ndiyo inayoburuta mkia, ilifungwa na Mtibwa katika mchezo wa ufunguzi, na jana imekutana na kipigo kingine kutoka kwa Lipuli FC.

Facebook Comments