Mabasi 9 yapigwa faini kwa mwendo kasi nyakati za usiku

Mabasi saba ya abiria yamekamatwa na kutozwa faini kwa kosa la mwendokasi na kutofuata sheria za usalama barabarani huku wakihatarisha maisha ya abiria.

Kamatakamata hiyo ambayo imesimamiwa na Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani, Fotunatus Muslim akiwa na timu ya viongozi na askari Mkoa wa Morogoro imefanyika usiku wa kuamkia leo, Jumamosi.

Zoezi la ukamataji mabasi hayo limefanyika eneo la Dumila, Wilaya ya Kilosa mkoani hapa, na lilichukua takribani saa mbili ambapo mabasi hayo yamezuiwa kuondoka hadi asubuhi huku yakitozwa faini.

Kamanda Muslim amesema jeshi hilo halitakubali kuona maisha ya watanzania yakipotea kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva.

Amesema kikosi hicho cha usalama barabarani kimeahidi kupambana na madereva wa mabasi ya abiria hususan nyakati za usiku kwani ndiyo wamekuwa wakiendesha kwa mwendokasi huku wakidai serikali muda huo inakuwa imelala.

Mabasi ya abiria zaidi ya saba yanayofanya safari kati ya mkoa wa Mara (Musoma), Dar es salaam na Mwanza – Dar es salaam yamekaguliwa na kutozwa faini.

Muslim amesema madereva wengi wamekuwa wakifuata sheria za barabarani nyakati za mchana kwa kuhofia kukamatwa kutokana na tochi zilizopo na inapofika nyakati za usiku madereva hao wamekuwa wakitumia mwanya huo kuendesha kwa mwendo kasi.

Akizungumzia dhamira ya Polisi, Muslim amesema ni kuwalinda raia na mali zao na kuwataka askari wa usalama barabarani kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

amesema operesheni hiyo ni endelevu na sasa itakuwa kwa nchi nzima kwa usiku na mchana huku akiwataka madereva hao kuacha kudanganyika kwa madai kuwa tochi usiku hazifanyi kazi.

“Nimekuja na slogani ya Kamata hii ni kwa wale madereva wasiotii na kufuata sheria na tutapambana nao kila wakati na nyakati zote na hiyo itasaidia abiria kusafiri salama na matumizi ya barabarani kuwa bora,” amesema kamanda Muslim

Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Leon Mwete, aliyekuwa katika moja ya basi yaliyokamatwa eneo hilo la Dumila amesema zoezi hilo ni zuri na linafaa kuendelea.

Amesema hii itapunguza ajali za barabarani na kwamba kwa sasa uendeshaji wa madereva wengi ni mzuri ukilinganisha na zamani.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*