Rooney akiri kosa afungiwa miaka miwili

Nahodha wa zamani wa Manchester United na Timu ya taifa ya England, Wayne Rooney amefungiwa kuendesha gari kwa muda wa miaka 2 baada ya kukiri kosa la kuendesha akiwa amelewa na kuomba radhi kwa kitendo hicho.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Jumatatu katika Mahakama ya Stockport nchini Uingereza ambapo pamoja na adhabu hiyo, pia imemtaka kulipa faini ya pauni 170 sawa na shilingi laki 5 za kitanzania, pamoja na kufanya shughuli za kijamii.

Mahakama hiyo imeeleza kuwa Rooney mwenye umri wa miaka 31 ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Everton, alikuwa amezidisha kilevi alichotumia mara tatu ya kiwango cha kawaida kinachoruhusiwa.

Rooney alikamatwa Septemba Mosi, mwaka huu ambapo baada ya kupimwa kiwango cha kilevi, alikutwa na microgramme 104 wakati kiwango cha juu kinachoruhusiwa nchini humo ni microgramme 35.

Facebook Comments