Vurugu zatikisa tena ligi daraja la kwanza

Vurugu zimezuka katika mchezo wa ligi daraja la kwanza kati ya timu ya JKT Mlale na Mawenzi Market uliopigwa mjini Morogoro.

Vurugu hizo zililazimu mchezo huo kusimama kwa muda ikiwa ni dakika ya 19 ya mchezo baada ya kiongozi wa JKT Mlale wakisaidiana na wenzao wa timu ya Mighty Elephant waliokuwepo uwanjani hapo, kumzuia mzee mmoja ambaye ni mlemavu asikae upande wa timu hiyo.

Baada ya dakika kadhaa za vurugu hizo, mchezo ukaendelea ambapo Mawenzi Market ya Morogoro ikakubali kichapo kingine kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya timu ya JKT Mlale kwa goli 1-0.

Bao la JKT Mlale limefungwa kwa mkwaju wa penati dakika ya 15 mara baada ya mchezaji wa timu hiyo kufanyiwa madhambi ndani ya boksi la 18.

Mawenzi imeendeleza wimbi la kutokuutumia uwanja wake wa nyumbani vyema ambapo sasa ina alama 3 kwa michezo minne huku timu ya JKT Mlale ikifikisha alama 1o kwa kucheza michezo minne pia.

Huu ni mchezo wa pili kukumbwa na vurugu za aina hiyo tangu kuanza kwa ligi hiyo Septemba 30 mwaka huu, ambapo mchezo wa kwanza ulikuwa ni kati ya Rhino Rangers na Alliance uliopigwa mjini Tabora.

Facebook Comments