Timu daraja la kwanza yaivimbia Yanga

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wamelazimishwa suluhu na timu ya daraja la kwanza la Kinondoni Municiple Council (KMC) katika mchezo wa kirafiki uliopigwa usiku wa leo katika dimba la Chamazi Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa ni maalum kwaajili ya vijana hao wa Jangwani kuchangisha fedha kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wao mazoezi maarufu kwa jina la Kaunda Stadium ulioko Jangwani jijini Dar es Salaam.

Mbali na lengo hilo, mchezo huo pia umetumika kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa Jumamosi ijayo katika dimba la Kaitaba mjini Bukoba.

Katika mchezo wa leo, kocha wa Yanga George Lwandamina amewapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao ni nadra kupata nafasi katika kikosi chake cha kwanza, akiwachanganya na wale waliozoeleka katika kikosi hicho hicho.

Baadhi ya waliopata nafasi leo ni pamoja na Festo Kaembe, Maka Edward, Matheo Anthony, Yusuph Mhilu, Baruan Akilimali, Mwinyi Haji na golikipa Benno Kakolanya ambao wamesaidiwa na Papy Kabamba, Andrew Vincent, Hassan Kessy, Juma Abdul na Geofrey Mwashiuya.

Ilikuwa ni mechi yenye burudani safi ikirushwa mbashara na Azam TV ambapo timu zote zimeonesha uimara huku zikisaka ushindi kwa kosa kosa za hapa na pale kutoka pande zote.

KMC pamoja na kuwa ni timu ya daraja la chini, imeonesha ushindani wa hali ya juu.

Facebook Comments