Majeruhi yamtibulia Lwandamina Yanga

KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, amesema wingi wa majeruhi kwenye kikosi chake
unampa wakati mgumu katika kipindi hiki wakijiandaa na michezo miwili ya ugeniniYanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, jana hakikufanya mazoezi baada ya kupewa mapumziko, na ina wachezaji wanne wa kikosi cha kwanza ambao ni majeruhi.

Nyota hao ni Obbrey Chirwa, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko pamoja na Amissi Tambwe.

Akizungumza na Nipashe jana, Lwandamina alisema anatamani kuona wachezaji wake wote wakiwa fiti kabla ya kukabiliana na Kagera Sugar mjini Bukoba.

“Lakini naamini baadhi yao wanaweza wakauwahi mchezo dhidi ya Kagera Sugar, ila kama kocha hali ya kuwa na majeruhi wengi inanichanganya,” alisema Lwandamina.

Alisema baada ya mchezo wa kirafiki wa juzi dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza ya KMC, aliamua kuwapumzisha kwa siku moja wachezaji wake na leo ataendelea na programu yake ya maandalizi kuelekea Bukoba.

Lwandamina alisema moja ya maeneo anayofanyia kazi kwenye kikosi chake ni safu yake ya ushambuliaji.

“Sifurahishwi na namna tunavyoshindwa kupata mabao, ni jambo ambalo naendelea kulifanyia kazi, ni lazima tutumie vizuri kila nafasi tunayoipata kwenye mchezo,” alisema.

Yanga inaondoka keshokutwa kuelekea Bukoba tayari kuwakabili Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba kabla ya kuelekea Shinyanga kuumana na Stand United Oktoba 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kambarage.

Yanga wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi tisa mbili nyuma ya vinara Simba

Facebook Comments