Mchezaji afungiwa kwa kumpiga mwamuzi

Mchezaji John Baraka anayechezea timu ya Area C inayoshiriki ligi daraja la pili, amesimamishwa kuendelea kucheza ligi hiyo kwa kosa la kumpiga ngumi mwamuzi ngumi ya mgongoni.

Adhabu hiyo imetolewa na kamati ya bodi ya ligi ya uendeshaji na usimamizi wa ligi katika kikao chake kilichopita baada ya kupitia taarifa na matukio mbalimbali yaliyojitokeza katika ligi hiyo ambapo pia mchezaji huyo alioneshwa kadi nyekundu kwa kosa hilo.

Taarifa ya kamati hiyo imesema kuwa mchezaji huyo alifanya kitendo hicho kwenye mechi namba moja ya kundi D la ligi daraja la pili kati ya Area C na Nyanza FC iliyofanyika Oktoba Mosi, mwaka huu kwenye uwanja wa Nyerere uliopo Mbulu mkoani Pwani.

“Kwa vile suala lake ni la kinidhamu, na kwa kutumia kanuni ya 9(5) ya ligi daraja la kwanza, kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi imemsimamisha kucheza mechi za ligi daraja la pili hadi suala lake litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Mchezaji wako atafahamishwa siku ambayo kikao cha kamati ya nidhamu kitafanyika kusikiliza shauri dhidi yake ambapo pia atapata fursa ya kuwasilisha utetezi wake kama upo.” Imesema sehemu ya barua iliyoandikiwa timu hiyo.

Facebook Comments