Simba yatambulisha kocha mpya

Klabu ya Simba leo Oktoba 19, 2017 imemtambulisha aliyekuwa kocha wa Rayon Sport ya Rwanda Masoud Djuma kuchukua nafasi ya Jackson Mayanja ambaye jana ametangaza kuachana na klabu hiyo.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Klabu ya Simba SC, Haji Manara mchana wa leo amemtangaza Masoud Djuma kuchukua nafasi ya kocha msaidizi katika klabu yao hiyo ya Simba na kuwaomba wanachama wa mashabiki wa Simba kumpa ushirikiano kocha huyo.

“Tunawaomba wanachama na mashabiki wa klabu ya Simba mumpe ushirikiano kocha wetu Masoud Djuma yeye ndiye atakuwa msaidizi wa Kocha Omog kuanzia leo Oktoba 19, 2017 na pia tumeboresha benchi la ufundi kwa kumteua meneja mpya Richard Robert yeye anachukua nafasi ya Dkt Kapinga ambaye alikuwa meneja kwa muda tuliokuwa naye mfupi lakini amerudi kwa mwajiri wake nasi klabu tumeona turidhie” alisema Haji Manara.

Mbali na hilo Manara amekanusha taarifa zinazoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kocha wao Mkuu Omog ameondoka klabuni hapo kwa sababu hajalipwa mshahara na kusema kuwa wao Simba hawajawahi kuwa na njaa na kusema kuwa kocha mkuu wao anaendelea na mazoezi na kikosi chao hivyo huo unaosambaa ni uzushi.

Facebook Comments