Kocha msaidizi mpya wa Simba asema haogopi kufukuzwa

Masudi Djuma raia na mchezaji wa baadhi ya timu nchini Burundi na Rwanda, amewasili leo, Alhamisi, Oktoba 19 kwa ajili ya kusaini mkataba wa kufundisha klabu ya Simba kama kocha msaidizi.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Burundi amewasili nchini siku moja baada ya aliyekuwa kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja kung’atuka rasmi jana.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)mjini Dar es Salaam, Juma alisema kwamba amekuja nchini kuwa kocha msaidizi wa Simba, chini ya Mcameroon, Joseph Marius Omog.

“Nimekuja kuwa kocha msaidizi wa Simba chini ya kocha aliyepo kwa sasa. Nataka kuisaidia Simba ifanikiwe kutwaa mataji zaidi najua hiyo ndiyo kiu kubwa,” amesema Juma ambaye mwaka 1995 aliichezea Burundi katika michuano ya Vijana ya Dunia ya FIFA nchini Qatar.

“Kazi ya ukocha ni ngumu, unaweza kufukuzwa wakati wowote, ndivyo ilivyo, hautakiwi kuwa na hofu. Lakini nitajitahidi kushirikiana na wenzangu kuhakikisha tunafanya vizuri.” alisema kocha huyo.

Mshambuliaji wa zamani wa Prince Louis ya Burundi, Inter Star za Burundi na Rayon Sport ya Rwanda amesema atafurahi iwapo atakuja kuifundisha Simba timu kubwa Afrika.

Historia ya ukocha kwa Juma inaanzia mwaka 2013 alipoanza kufundisha timu za vijana za kwao, Burundi kufuatia kustaafu soka mwaka 2010 akiwa na klabu ya Inter Star ya nchini humo aliyojiunga nayo akitokea Rayon Sport ya Rwanda mwaka 2009.

Juma mwenye umri wa miaka 40 ambaye alitua Rayon mwaka 2003 alipojiunga nayo akitokea Prince Louis ya kwao, baada ya kazi nzuri na timu za taifa za vijana za Burundi alirejea Kigali Desemba mwaka 2010 kujiunga na The Blues kama kocha msaidizi akichukua nafasi ya Sosthene Habimana, aliyehamia Sunrise FC, chini ya Mbelgiji, Ivan Minneart.

Juma akateuliwa kuwa kaimu kocha mkuu wa Rayon, Februari mwaka jana kufuatia kuondoka kwa Mbelgiji Minneart, hadi mwishoni mwa msimu wa 2015/2016.

Katika kipindi chake cha kuwa kocha mkuu wa Rayon, aliiongoza timu hiyo kutwaa Kombe la Amani kwa mara ya tisa ya rekodi na kwa mara ya kwanza baada ya karibu miaka 11, hivyo kuiwezesha kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika ambako walifika kwenye hatua ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi.

Kocha msaidizi mpya wa Simba, Masoud Djuma amesema anapenda changamoto mpya lakini si mwoga kufukuzwa.

Facebook Comments