Niyonzima awapa neno ‘tamu’ Simba

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Niyonzima, alisema kuwa mashabiki wengi wamekuwa wakihoji kiwango chake cha sasa wengi wakiona kama hayupo kwenye kiwango chake kinachofahamika.

“Mashabiki wawe wavumilivu, inawezekana sijawa kwenye kiwango walichokizoea, lakini wakumbuke nilikosa sehemu kubwa ya maandalizi kwa ajili ya msimu mpya (Pre Season),” alisema Niyonzima.

Alisema kwa muda sasa amekuwa kwenye prograumu maalum aliyopewa na kocha wa timu hiyo ili kurejea kwenye makali yake na anaamini wiki mbili zijazo atakuwa kwenye ubora wake.

“Kwa wale wanaojua mpira wanafahamu nazungumza nini na hawawezi kunilaumu, ligi bado mbichi hata michezo 10 hatujafikisha, naamini baada ya muda nitarejea kwenye makali waliyoyazoea,” alisema Niyonzima.

Aidha, Niyonzima, alisema ligi msimu huu ni ngumu na yenye ushindani mkubwa na hiyo ni kutokana na timu kujiandaa vyema.

“Nafikiri na kingine ni kuanza kuja wadhamini kwa wingi kwenye klabu mbalimbali kumeongeza ushindani, tulizoea kuona klabu za Simba, Yanga na Azam kuwa na wadhamini, lakini kwa sasa unaweza kuona wadhamini wanajitokeza kwa timu nyingine kama Singida United, Mbao na nyingine,” alisema Niyonzima.

Facebook Comments