Rekodi za Simba na Yanga kuelekea mchezo wa leo

Tangu kuanza kwa msimu wa 2017/18 ligi kuu soka Tanzania bara, watani wa jadi Yanga na Simba wanaonekana kufungana kwenye kila jambo ambapo rekodi pekee inayowafanya watofautiane ni idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kuelekea mchezo wa leo hizi ndio rekodi mbalimbali za Yanga na Simba kwenye mechi saba za ligi kuu ambapo timu zote mbili zina alama 15.

Baada ya mechi hizo saba timu zote zimeshinda mechi 4 ambazo ni jumla ya alama 12 pamoja na sare 3 ambazo zimezalisha alama 3 hivyo kukamilisha alama 15 ambazo timu hizo zimejikusanyia kabla ya mchezo wa leo.

Pia timu zote mbili hazijapoteza mchezo hata mmoja, wakati upande wa mabao ya kufungwa klabu ya Yanga imeruhusu mabao 3 huku Simba ikiwa imeruhusu mabao 4. Mabao ya kufunga Simba imefunga mabao 19 huku Yanga ikiwa imefunga mabao 10.

Washambuliaji Ibrahim Ajibu wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba ndio wanaongoza orodha ya kufumania nyavu msimu huu. Okwi ana mabao 8 huku Ajibu akiwa na mabao 5. Je nani leo ataongeza akaunti ya mabao?

Facebook Comments