ACT yaitupia polisi lawama kwa hili.

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema tangu Chama chao kuingia kwenye matatizo ya Polisi siku za karibuni zimeathiri kwa sehemu kubwa ushiriki wao kama chama kwenye Kampeni za marudio ya uchaguzi wa madiwani.

Ndg Shaibu amesema hayo kwenye taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari ambapo amesema kwamba kama jeshi la polisi litataka kuwahoji viongozi wa chama chao basi litapaswa kutengeneza utaratibu ambao hauathiri ushiriki wao wa kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi huu.

Aidha amesema kwamba Kaimu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Dorothy Semu leo aliitikia wito wa jeshi la Polisi (Kituo cha Makosa ya Kifedha, Kamata, Dar es salaam) kama walivyomtaka kwenda kutoa maelezo ya ziada kuhusu nyaraka na vifaa vya kieletroniki vilivyochukuliwa kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Chama siku ya Jumanne wiki hii.

“Kama tulivyoeleza huko awali, danadana hizi za Jeshi la polisi zimeathiri kwa sehemu kubwa ushiriki wetu kwenye Kampeni za marudio ya uchaguzi wa madiwani. Kama jeshi la polisi litataka kuwahoji viongozi wetu litapaswa kutengeneza utaratibu ambao hauathiri ushiriki wetu wa Kampeni. ” Ndg Shaibu

Ameweka wazi kuhusu kampeni za Uchaguzi kwamba Kaimu Mwenyekiti wa Chama Ndugu Yeremia Kulwa Maganja anatarajiwa kufanya ziara kwenye mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kushiriki ufunguzi wa Kampeni kwenye kata zilizopo kwenye mikoa hiyo ambazo zinarudia uchaguzi.

Ikumbukwe kuwa juzi tarehe 7 Novemba 2017 Jeshi la Polisi lilifanya upekuzi katika Makao Makuu ya ACT Wazalendo yaliyopo Kijitonyama Jijini Dar es salaam na kuondoka na nyaraka za chama kuhusu Kusinyaa kwa uchumi wa nchi na vifaa vya kielektroniki (flash na laptop) vilivyotumika kuandaa taarifa hizo za kiuchambuzi.

Facebook Comments