Magufuli aahidi kuyafanyia kazi maoni ya Watanzania waishio nje ya nchi

Rais John Magufuli amewahakikishia Watanzania waishio nchini Uganda katika Mji wa Masaka kuwa atayafanyia kazi maoni yao kwa kushirikiana na mawaziri wake waliojibu hoja mbalimbali na kuwataka kutosita kuwasilisha maoni yao kwa serikali.

Katika mkutano huo rais Magufuli, aliwaeleza Watanzania hao kuhusu hatua zilizoanza kuchukuliwa na serikali yake katika kuleta mabadiliko ambazo zimeanza kuzaa matunda.

Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe Janeth Magufuli, mawaziri na viongozi wakuu wa taasisi za serikali ametaja baadhi ya matokeo hayo kuwa ni pamoja na usimamiaji mzuri wa uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia 7, kudhibiti mfumuko wa bei hadi asilimia 5.1, kuokoa shilingi bilioni 238 walizokuwa wanalipwa watumishi hewa kwa mwaka na kuondoa watumishi wenye vyeti feki waliokuwa wakilipwa takribani shilingi bilioni 142 kwa mwaka.

Matokeo mengine ni kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi bilioni 850 hadi wastani wa shilingi trilioni 1.2 kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726 ambapo shilingi trilioni 7 zitatumika, kununua ndege 6 za serikali kwa ajili ya kuinua utalii na kuimarisha usafiri wa anga, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi 269.

Rais Magufuli pia amesema serikali imechukua hatua madhubuti za kuwavutia wawekezaji na sasa wengi wapo katika hatua mbalimbali za uwekezaji ikiwemo ujenzi wa viwanda na ametoa wito kwa watanzania hao kuendelea kuwashawishi wawekezaji wengine kwenda kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa fursa zipo nyingi.

Katika mkutano huo Watanzania waishio Uganda wamemshukuru na kumpongeza rais Magufuli kwa juhudi mbalimbali anazozifanya na wameomba serikali iwajengee mazingira bora pale wanapowapeleka wawekezaji nchini Tanzania.

Huu ni mkutano wa kwanza wa rais Magufuli kukutana na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) na Uganda kuna Watanzania 45,000 waishio nchini hapa.

Facebook Comments